Ethiopia yamteua mwanamke mpinzani kuongoza Tume ya Uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49686-ethiopia_yamteua_mwanamke_mpinzani_kuongoza_tume_ya_uchaguzi
Bunge la Ethiopia limemuidhinisha kiongozi mashuhuri wa upinzani aliyekuwa akiishi uhamishoni, Birtukan Mideksa kuwa mkuu mpya wa Tume ya Uchaguzi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2018 11:27 UTC
  • Ethiopia yamteua mwanamke mpinzani kuongoza Tume ya Uchaguzi

Bunge la Ethiopia limemuidhinisha kiongozi mashuhuri wa upinzani aliyekuwa akiishi uhamishoni, Birtukan Mideksa kuwa mkuu mpya wa Tume ya Uchaguzi nchini humo.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmed Abey amemtaja mwanasiasa huyo aliyerejea nchini Ethiopia wiki chache zilizopita akitokea Marekani, kuwa ni shakhsia anayeheshimu mfumo wa sheria, huru na asiyeegemea upande wowote, na ni mwenye kuamini juu ya usawa kwa Waethiopia wote.

Mwanamama huyo amekuwa na nyadhifa tofauti katika vyama mbalimbali vya upinzani nchini humo, vikiwemo vya Unity for Democracy and Justice (UDJ), Rainbow Ethiopia, Movement for Democracy and Social Justice na Coalition for Unity and Democracy.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Ahmed Abey

Kuteuliwa kwake ni katika mlolongo wa mageuzi na mabadiliko makubwa yanayofanywa na serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmed Abey, tangu aingie madarakani mwezi Aprili mwaka huu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Ethiopia ilimteua mwandiplomasia wa kimataifa, Sahle-Work Zewde kuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wiki moja kabla ya uteuzi wa Sahle-Work ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu katika Umoja wa Afrika, AU, Abey alilifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na kuwateua wanawake 10 kuwa mawaziri, na kuifanya nchi hiyo iwe ya tatu baada ya Rwanda na Ushelisheli, kuwa na baraza la mawaziri lenye asilimia 50 ya mawaziri wanawake barani Afrika.