Wapinzani kuandamana dhidi ya serikali nchini Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49793-wapinzani_kuandamana_dhidi_ya_serikali_nchini_zimbabwe
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimetangaza Alkhamisi ya kesho kutwa kuwa siku ya kufanya maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 27, 2018 08:01 UTC
  • Wapinzani kuandamana dhidi ya serikali nchini Zimbabwe

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimetangaza Alkhamisi ya kesho kutwa kuwa siku ya kufanya maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali.

Msemaji wa chama cha MDC, Jacob Mafume amesema tayari wameitaarifu polisi ya nchi hiyo kuhusu maandamano hayo, yatakayofanyika kwa ajili ya kulalamikia mfumuko wa bei za bidhaa na kudorora kwa uchumi wa nchi hiyo.

Mapema mwezi huu, Nelson Chamisa, kinara wa chama hicho cha upinzani alisema maandamano yajayo ya nchi nzima ya wapinzani yatakuwa mwanzo wa kuishinikiza serikali iliyoko mamlakani kuachia ngazi, na upinzani kutwaa madaraka.

Awali Chamisa alitoa mwito wa kuundwa Mamlaka ya Kitaifa ya Mpito nchini humo, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro kuhusu uhalali wa serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa, mwito ambao serikali iliutaja kama njama za kuingia madarakani kupitia mlango wa nyuma.

Nelson Chamisa, kinara wa MDC

Kiongozi huyo wa upinzani ambaye chama chake kimekataa kata kata kutambua ushindi wa Mnangagwa katika uchaguzi wa urais wa Julai 30, amesema serikali ambayo sio halali haina uwezo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye ametoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya vyama vya siasa kwa ajili ya kujenga upya uchumi wa nchi hiyo, anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukomesha hali ya kutengwa Zimbabwe kimataifa na kurekebisha uchumi unaoyumbayumba kutokana na ukosefu wa ajira na uhaba wa fedha za kigeni.