Mkutano wa Matumizi Endelevu ya Bahari waendelea Nairobi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49805-mkutano_wa_matumizi_endelevu_ya_bahari_waendelea_nairobi
Mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi endelevu ya bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi umeingia siku ya pili hii leo huko Nairobi, Kenya, huku washiriki wakizungumzia umuhimu wa bahari katika uchumi wa visiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 27, 2018 11:42 UTC
  • Mkutano wa Matumizi Endelevu ya Bahari waendelea Nairobi

Mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi endelevu ya bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi umeingia siku ya pili hii leo huko Nairobi, Kenya, huku washiriki wakizungumzia umuhimu wa bahari katika uchumi wa visiwa.

Washiriki wa mkutano huo wanaangazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuwa na maeneo yaliyotengwa ya baharini kwa ajili ya matumizi endelevu ya bahari.

Mkutano huo ulianza jana Jumatatu na leo Rais Uhuru Kenyatta alihutubia wajumbe kutoka mataifa 180. Katika hotuba yake Rais Kenyatta alisema zaidi ya watu bilioni 2.5 wanakabiliwa na changamoto ya mazingira machafu kote duniani. 

Hata hivyo Rais Kenyatta anasema kuna faida nyingi zitokanazo na miji iliyokaribu na bahari, kama vile usafirishaji wa mizigo kutoka taifa moja hadi lingine kupitia bandari za mataifa hayo, na ameyahimiza mataifa yenye bahari kuitunza vyema raslimali hiyo.

Kando na hayo  Rais Kenyatta wa Kenya amehimiza ulimwengu kuweka mikakati ya kuzuia uchafuzi wa mazingira, sawia na kuweka mipango thabiti ya kuendeleza ukuaji wa miji kupitia miundo msingi ya kisasa bila kuharibu mazingira.

Kati ya viongozi wanaoshiriki ni marais wa Ushelisheli, Namibia, Uganda, Jamhuri ya Kongo, Somalia na Fiji. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein tayari yuko Kenya kuhudhuria mkutano huo wa Uchumi wa Bahari, ambapo anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Inakadiriwa zaidi ya wajumbe 15,000 wanashiriki katika mkutano huo wa Nairobi ambao ni wa kwanza wa aina yake duniani.