Nov 30, 2018 06:22 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram Nigeria sasa watumia droni na wapiganaji wa kigeni

Magaidi wakufurishaji wa kundi Boko Haram nchini Nigeria sasa wanatumia ndege zisizo na rubani au droni katika kufanya hujuma zao za kigaidi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mkuu wa jeshi la Nigeria Jenerali Tukur Buratai amesema kwenye taarifa yake kuwa, katika miezi miwili au mitatu iliyopita, wameshuhudia ongezeko la matumizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya jeshi la Nigeria. Aidha amesema idadi kubwa ya magaidi wa kigeni wanaendelea kujiunga na kundi la Boko Haram.

Amesema kati ya Novemba 1 na 18 mwaka huu, kundi hilo limefanya mashambulizi matano dhidi ya jeshi, lakini mashambulizi hayo yalizimwa.

Umoja wa Mataifa umesema kundi hilo linasababisha changamoto kubwa ya usalama, hali ya kibinadamu na utawala.

Hivi sasa kundi hilo limekuwa likiendesha vitendo vya kigaidi katika nchi za Cameroon, Chad, Niger na Nigeria, na mpaka sasa limeshapelekea watu zaidi ya milioni 2.4 kwenye eneo za Ziwa Chad wakimbie makazi yao.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009.

Boko Haram ni kundi linalofuata itikadi za Kiwahhabi na limeitumbukiza Nigeria katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha mizozo ya kidini na kikabila nchini humo.

 

Tags