Umuhimu wa mkutano wa Ofisi za Kieneo za Kuususia Utawala wa Kizayuni
Mkutano wa 92 wa Ofisi za Kieneo za Kuususia Utawala wa Kizayuni umefanyika katika makao makuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo Misri na kushirikishwa wawakilishi kutoka nchi za Kiarabu na wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.
Hatua ya Jumuia ya Nchi za Kiarabu ya kuitisha mkutano huo kunalifanya jambo hilo kuwa na umuhimu kadhaa. Kwanza ni kwamba mkutano huo unaonesha kuwa, ijapokuwa baadhi ya nchi za Kiarabu zilizojiingiza kwenye mkondo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini mtazamo mkuu wa ulimwengu wa Kiarabu ni kupinga siasa za nchi hizo na ni kuliunga mkono taifa la Palestina suala ambalo linahesabiwa kuwa na ni kitu cha thamani kubwa katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na wa Kiarabu. Kwa hakika, kufanyika mkutano huo ulioshirikisha wajumbe kutoka nchi za Kiarabu ni uthibitisho kwamba njama za kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel siyo fikra na wala sio msimamo ya ulimwengu wa Kiarabu.
Nukta ya pili ni kwamba mkutano huo umefanyika katika mazingira ambayo hivi karibuni Israel ilishindwa vibaya katika vita ilivyovianzisha dhidi ya muqawama wa Palestina na hadi hivi sasa hasara za kushindwa huko zinaendelea kuuelemea utawala wa Kizayuni mbali na kujiuzulu waziri wa vita wa utawala huo na kuwekwa chini ya mashinikizo makubwa serikali ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel. Kwa kuzingatia hali hiyo tutaona kuwa, hatua yoyote ya kuliunga mkono taifa la Palestina hivi sasa hata kwa maneno na fikra tu kama hivyo kuitisha mkutano kama huo wa mjini Cairo ni kwa faida ya wananchi wa Palestina.
Tatu ni kwamba, Mkutano wa 92 wa Ofisi za Kieneo za Kuususia Utawala wa Kizayuni umefanika huko Cairo kwa ajili ya kupinga jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi hivi sasa, wananchi wa Palestina wamekuwa wakifanya maandamano ya haki ya kurejea kila siku ya Ijumaa na huu ni mwezi wa tisa tangu kuanza maandamano hayo. Pamoja na kwamba maandamano hayo ni ya amani, lakini utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya jinai za kila namna kujaribu kuyakandamiza kiasi kwamba kwa mujibu wa takwimu za kituo cha mjini Quds cha utafiti wa masuala ya Kizayuni na Palestina, Wapalestina 211 wameshauwa shahidi na wengine zaidi ya 17 elfu wameshajeruhiwa tangu mwezi Machi hadi hivi sasa. Hivyo kufanyika mkutano wa kuisusia Israel huko nchini Misri ni sawa na kutangaza kupinga jinai hizo za Israel na kuunga mkono muqawama wa wananchi wa Palestina.
Nukta ya nne ni kuwa, vikwazo vya namna hiyo kimsingi vina sura ya kiuchumi na ni hatua ya kisheria ya kulinda ahadi za kimataifa za kulitetea taifa la Palestina. Mikutano ya namna hiyo ambayo matunda yake yanatakiwa yawe ni kususiwa bidhaa za Israel inaweza sambamba na kuuletea madhara ya kiuchumi utawala wa Kizayuni, inaweza pia kupunguza kasi ya harakati za baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu za kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel. Said Abu Ali, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika masuala ya Palestina amesema kuwa, mkutano huo wa Cairo ni aina moja ya muqawama wa amani wa kupigania haki za Palestina.
Nukta ya tano ni kwamba mkutano huo umefanyika katika hali ambayo kususiwa bidhaa za Israel ni harakati ya dunia nzima hivi sasa. Harakati ya kimataifa ya kuisusia Israel inayojulikana kwa jina la BDS ambacho ni kifupisho cha Boycott Divestment Sanction ilianza mwaka 2005 kwa lengo la kukomesha kukoloniwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kutambuliwa haki za kimsingi za taifa hilo madhlumu.
Harakati za BDS zilipata nguvu zaidi kuanzia mwezi Disemba 2017 baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa eti Baytul Muqaddas ni mji mkuu wa Israel. Hivyo kufanyika Mkutano wa Ofisi za Kieneo za Kuususia Utawala wa Kizayuni huko Cairo Misri ni uendelezaji wa harakati ya kimataifa na ya dunia nzima dhidi ya utawala wa Kizayuni na kupinga mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne."