Mahakama Zambia yamuidhinisha Rais Lungu kugombea muhula wa tatu
Mahakama ya Katiba Zambia imetangaza kuwa Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo anaweza kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu ujao unaotazamiwa kufanyika mwaka 2021.
Rais wa Mahakama ya Katiba ya Zambia, Hildah Chibomba amesema majaji wote saba wa mahakama hiyo wameidhinisha kwa kauli moja ombi la vyama vinne vya upinzani vilivyoitaka mahakama hiyo itangaze kuwa Lungu anaruhusiwa kisheria kuwania muhula wa tatu.
Majaji hao wamesema kipindi cha kwanza cha Rais Lungu kuwa madarakani hakiwezi kuhesabiwa kuwa muhula kamili wa uongozi kwani katiba ya nchi inasema muhula kamili ni kuanzia miaka mitatu hadi mitano.
Lungu alichanguliwa kuwa rais wa Zambia kwa mara ya kwanza Januari mwaka 2015, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Michael Sata, na kisha kuongoza kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita, kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika Septemba mwaka 2016.
Vyama vya upinzani tayari vimekosoa vikali azma ya Lungu ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2021 kwa muhula wa tatu, kwani kisheria, hafai kuwania urais kwa zaidi ya vipindi viwili.
Mwezi Machi mwaka huu, azma ya chama kikuu cha upinzani nchini Zambia cha UPND cha kuwasilisha hoja bungeni kwa shabaha ya kumsaili na kumuuzulu Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo iligonga mwamba.
Itakumbukwa kuwa, Rais Lungu, alimshinda kinara wa chama cha upizani cha UPND, Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa mwaka juzi uliokuwa na ushindani mkali. Hata hivyo Hichelema alikataa kumtambua Lungu kama rais wa Zambia na kusema kura zake ziliibwa.