Viongozi wa Sudan Kusini watoa mwito kwa wananchi kusameheana
-
Rais Salva Keer wa Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na naibu wake Wani Igga wanaendeleza kampeni ya pamoja wakitaka kuwaunganisha na kuwapatanisha watu wa Sudan Kusini waliosambaratika kutokana na vita vikali vya miaka mitano.
Kwenye ujumbe wao uliorushwa kwenye redio za nchi hiyo, viongozi hao wamewasihi watu wa Sudan Kusini kusameheana ili kuweka njia ya mapatano katika taifa zima. Kwenye kampeni hiyo inayoongozwa na makundi ya kidini, yanatumika mabango na rikodi ili kueneza ujumbe wa amani nchi nzima.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Nchi hiyo ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Hivi karibuni pande hasimu zilifikia mapatano ya amani na inatarajiwa kuwa utulivu utarejea nchini humo.