Polisi ya Kongo yafyatua risasi hai kutawanya wafuasi wa mgombea wa upinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50141-polisi_ya_kongo_yafyatua_risasi_hai_kutawanya_wafuasi_wa_mgombea_wa_upinzani
Polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana kwa siku ya pili mfululizo walitumia gesi ya kutoa machozi na kuwafyatulia risasi hai wafuasi wa Martin Fayulu mgombea wa upande wa upinzani ili kuwatawanya na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2018 04:47 UTC
  • Polisi ya Kongo yafyatua risasi hai kutawanya wafuasi wa mgombea wa upinzani

Polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana kwa siku ya pili mfululizo walitumia gesi ya kutoa machozi na kuwafyatulia risasi hai wafuasi wa Martin Fayulu mgombea wa upande wa upinzani ili kuwatawanya na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Kampeni za uchaguzi wa Kongo unaosubiriwa kwa hamu uliopangwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikifanyika kwa amani na utulivu, lakini kuibuka ghasia za hapa na pale katika mkoa wa Katanga kusini mashariki mwa nchi hiyo kumezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kukaririwa machafuko kama yale yaliyoshuhudiwa katika chaguzi za mwaka 2006 na 2011 nchini humo.

Polisi katika mji wa Kalemie jana walizuia magari yaliyokuwa katika msafara wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu uliokuwa ukielekea katika mkutano wa kampeni na kuanza kufyatua risasi angani. Mwanamke mmoja alipigwa risasi na kuaaga dunia na Rogatien Kitenge kiongozi wa taasisi ya kiraia ameathibitisha kuwa polisi wa Kongo walifyarua risasi hai na kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi wafuasi wa mgombea huyo wa upinzani. Amesema kwamba mwanamke mmoja alipoteza maisha.

Martin Fayulu alifanya mkutano wake wa kampeni licha ya kukabiliana na polisi. Msemaji wa serikali na polisi ya Kongo hawakuweza kupatikana kutoa maelezo kuhusu suala hilo. Fayulu ni mmoja kati ya viongozi wawili wa upinzani wanaochuana na Emmanuel Ramazan Shadary, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye anauwakilisha muungano wa chama tawala kinachoongozwa na Rais Joseph Kabila.

Martin Fayulu, mmoja wa wagombea wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Kongo 

Kabila hawezi tena kugombea kiti cha rais baada ya mihula yake kumalizika. Joseph Kabila amekuwa madarakani kwa miaka 18.