Machafuko Niger yapelekea watu 52,000 kuwa wakimbizi
Machafuko katika maeneo ya mpaka wa Niger na nchi za Mali na Burkina Faso yamepelekea raia 52,000 wa Niger kuwa wakimbizi mwaka huu wa 2018.
Hayo yamedokezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ambalo limesema mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanamgambo kwenye maeneo ya mpakani ya Niger ya Tillaberi na Tahoua, yamesababisha watu wengi kusaka maeneo salama kwenye miji na vijii vya karibu.
Raia wanaokimbia machafuko wanaeleza kuwa makundi ya watu wenye silaha wanaripotiwa kushambulia vijiji, kuua na kuteka nyara raia wa kawaida, wakiwemo viongozi wa kijamii, huku wakichoma moto shule na pia kupora mali kutoka nyumba za watu, biashara na pia mifugo.
Licha ya hali ya hatari iliyotangazwa na serikali ya Niger katika maeneo ya mpakani ya Tahoua na Tillaberi ikiendelea na kuwepo kwa idadi kubwa ya vikosi vya Sahel kutoka nchi tano au G5, bado ukosefu wa usalama pamoja na machafuko yanazidi kukwamisha juhudi za kutoa misaada ya kibinadamu.
Kundi la nchi za G5 za eneo la Sahel Afrika linalojumuisha nchi za Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad limetangaza hivi karaibuni kuwa liliafiki kuanzishwa operesheni kubwa dhidi ya makundi ya kigaidi na wabeba silaha katika eneo hilo.