Uchaguzi Mkuu DRC waahirishwa, sasa kufanyika Disemba 30
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50326-uchaguzi_mkuu_drc_waahirishwa_sasa_kufanyika_disemba_30
Tume ya Uchaguzi ya Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo (CENI) imetangaza kuwa uchaguzi mkuu uliokuwa umepangiwa kufanyika Jumapili Desemba 23 sasa umeahirishwa hadi Jumapili Disemba 30, 2018.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2018 13:27 UTC
  • Uchaguzi Mkuu DRC waahirishwa, sasa kufanyika Disemba 30

Tume ya Uchaguzi ya Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo (CENI) imetangaza kuwa uchaguzi mkuu uliokuwa umepangiwa kufanyika Jumapili Desemba 23 sasa umeahirishwa hadi Jumapili Disemba 30, 2018.

Mwenyekiti wa tume Corneille Nangaa ametangza kwamba uamuzi huo umechukuliwa baada ya ghala la CENI kuteketea kwa moto wiki iliyopita katika mji mkuu, Kinshasa. Moto huo uliteketeza asilimia 80 ya vifaa vyote vya kupigia kura.  CENI inasema baada ya kuandaa kikao na wawakilishi wa vyama vya kisiasa waliamua kuchukuwa uamzi wa kuakhirisha uchaguzi hadi Disemba 30.

Mwenyekiti wa Ceni amesema kabla ya kuchukuwa uamuzi huo, walikubaliana na wanasiasa mbalimbali kuakhirisha uchaguzi kwa wiki moja ili waweze kupata vifaa vya uchaguzi kwa mkoa wa Kinshasa.

Emmanuel Ramazani Shadary

 

Corneille Nangaa amesema uchaguzi hauwezi kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini DRC bila kuwemo mkoa wa Kinshasa ambao ulipoteza vifaa vya uchaguzi, baada ya ghala moja kuu lililokuwa likihifadhi vifaa hivyo kuteketea kwa moto.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamekosoa hatua hiyo, huku upinzani ukitarajia kutoa msimamo wake rasmi baadaye.

Katika uchaguzi huo ulioahirishwa, mgombea urais Emmanuel Ramazani Shadary anayeungwa mkono na Rais Joseph  Kabila anayeondoka madarakani anatarajiwa kukabiliwa na kibarua kigumu kutoka kwa wapinzani wake wawili Felix Tshisekedi na Martin Fayulu.