Watu 27 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani Kongo DR
(last modified Tue, 25 Dec 2018 14:30:20 GMT )
Dec 25, 2018 14:30 UTC
  • Watu 27 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani Kongo DR

Watu wsiopungua 27 wameaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea magharibi mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa.

Dakta Sylvain Yuma, ofisa wa Wizara ya Afya wa DRC amesema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia leo, magharibi mwa Kinshasa, ambapo basi la abiria lilipoteza mwelekeo na kugongana ana kwa ana na lori.

Amesema watu wengine 17 wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Kisantu mkoani Kongo-Centra, na kwamba sita miongoni mwao wako katika hali mahututi.

Malori mawili yaligongana mwezi Oktoba mwaka huu katika kijiji kimoja kilichoko karibu na eneo hilo la Kisantu, na kupelekea watu 53 kupoteza maisha.

Ramani ya DRC

Katika hatua nyingine, wanajeshi 15 wa Kongo DR wamejeruhiwa baada ya ndege iliyokuwa imewabeba kupata hitilafu wakati wa kutua katika mji wa Beni, mashariki mwa nchi jana Jumatatu.

Ofisa mkuu wa usalama katika Uwanja wa Ndege wa Beni, Luteni Somwe Mulimbi amesema ndege hiyo ilikuwa imebeba watu 68, na kwamba askari 15 walipata majeraha mabaya, lakini kwa sasa wanaendelea kutibiwa.