Watu 27 wauawa na kujeruhiwa katika mapigano mapya kusini mwa Libya
Kundi moja lenye silaha limevamia kituo kimoja cha askari wanaoitwa Jeshi la Taifa la Libya kusini mwa nchi hiyo na kupelekea kuuawa na kujeruhi watu 27.
Mtandao wa habari wa al Wasat wa Libya umetangaza habari hiyo na kusema kuwa, kundi hilo lilitokea nchini Chad jana Alkhamisi na kushambulia askari hao wa Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar katika eneo la Traghan la kusini mwa Libya.
Watu saba wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika uvamizi huo ambao umepelekea pia kufungwa mashule katika eneo hilo na watu kujificha na kutojitokeza mitaani.
Ripoti zinasema kuwa, makundi yenye silaha yakiwemo wa nchini Chad yana maficho yao katika eneo la Umm al Aranib la kusini mwa Libya.
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kuwa na utulivu wa hata siku moja tangu mwaka 2011 wakati Marekani ilipoivamia kijeshi Libya ikiongoza jeshi la nchi za Magharibi NATO.
Baada ya madola hayo ya Magharibi kuivamia kijeshi Libya na kufanya uharibifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kulivunja jeshi, yaliitelekeza nchi hiyo huku silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa makundi chungu nzima hasimu ambayo kila moja linatumia silaha hivi sasa kupigania kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo.