Martin Fayulu, mgombea wa upinzani aongoza katika kura ya maoni DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50479-martin_fayulu_mgombea_wa_upinzani_aongoza_katika_kura_ya_maoni_drc
Utafiti mpya wa maoni umeonesha kuwa mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Fayulu ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Jumapili ijayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2018 12:34 UTC
  • Martin Fayulu, mgombea wa upinzani aongoza katika kura ya maoni DRC

Utafiti mpya wa maoni umeonesha kuwa mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Fayulu ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Jumapili ijayo.

Katika taarifa ya leo Ijumaa, taasisi ya utafiti ya Congo Research Group (CRG), yenye makao yake mjini New York imesema iwapo uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki, basi Fayulu ataibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 44 ya kura, akifuatiwa na mgombea mwingine wa upinzani, Felix Tshisekedi, kinara wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kwa asilimia 23.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa maoni, mgombea wa chama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary aliyependekezwa na Rais Joseph Kabila kupeperusha bendera ya chama tawala na ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo ataibuka wa tatu katika uchaguzi huo kwa asilimia 18.

Martin Fayulu, mwenye umri wa miaka 61, si maarufu katika siasa ndani na nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini alikuwa mstari wa mbele katika maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa nchini humo DRC tangu mwaka 2015 na kuonekana mmoja kati ya watu waliompinga Kabila kuwania  muhula wa tatu.

Fayulu (kushoto) na Felix Tshisekedi

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya umelaani kitendo cha serikali ya DRC kumfukuza Balozi wake nchini humo, na kusisitiza kuwa hatua hiyo haikubaliki na haikupaswa kuchukuliwa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Kongo DR, Leonard She Okitundu amesema Balozi huyo wa EU huyo Bart Ouvry, raia wa Ubelgiji ana saa 48 kuondoka nchini humo, uamuzi uliochukuliwa siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa Jumapili.