Wapinzani Kongo DR walalamikia ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50538-wapinzani_kongo_dr_walalamikia_ukiukwaji_mkubwa_wa_taratibu_katika_uchaguzi_wa_rais
Wagombea wakuu wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamedai kuwa uchaguzi wa jana Jumapili ulikumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo za kukwama kwa mashine za kupigia kura, mvua kubwa katika maeneo mengi pamoja na machafuko na vurugu.
(last modified 2026-02-25T11:30:13+00:00 )
Dec 31, 2018 08:05 UTC
  • Wapinzani Kongo DR walalamikia ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika uchaguzi wa rais

Wagombea wakuu wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamedai kuwa uchaguzi wa jana Jumapili ulikumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo za kukwama kwa mashine za kupigia kura, mvua kubwa katika maeneo mengi pamoja na machafuko na vurugu.

Felix Tsishekedi, mmoja wa wagombea wanaopewa nafasi ya kushinda urais, amesema inaovyoonekana Rais Joseph Kabila anaweza kuendelea kubaki madarakani, ikiwa uchaguzi utafutwa kutokana na hitilafu zilizobainika.

''Mambo yamevurugika kiasi kwamba tunashuku pengine ni vurugu za kupangwa, kwa makusudi ya kuipa Mahakama ya Katiba kisingizio cha kuufuta uchaguzi huu kesho.'' alilalamikaTshisekedi hapo jana.

Taasisi ya Mkutano wa Maaskofu wa Kikatoliki (CENCO), ambayo ni miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi huo imesema mashine za kupigia kura ambazo tangu mwanzo zililalamikiwa na upinzani zilikwama katika vituo 544 kati ya 12,300 walivyovikagua katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Moja ya matukio ya machafuko yaliyoripotiwa katika uchaguzi wa jana lilitokea katika kituo kimoja cha kupigia kura katika jimbo la Kivu ya Kusini, mashariki mwa nchi, ambapo polisi alimpiga risasi na kumuua kijana mmoja baada ya kuzozana kuhusu madai ya kufanywa udanganyifu katika zoezi la upigaji kura.

Imeelezwa kuwa umati wa watu waliokuwepo katika eneo hilo walilipiza kisasi kwa kumpiga polisi huyo hadi kufa. Hayo yamethibitishwa na mashahidi na wanasiasa waliokuwepo mahali hapo. Katika ghasia hizo, afisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) pia aliuawa.

Uchaguzi ni tukio la nadra nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa mkoloni Mbelgiji imeshuhudia utawala wa kidikteta, mauaji ya kisiasa, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Joseph Kabila akipiga kura katika uchaguzi wa Desemba 30

Ikiwa Rais Kabila ambaye amekuwako madarakani tangu kuuawa baba yake Laurent Desire Kabila mwaka 2001 ataondoka madarakani baada ya uchaguzi huo, itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kubadilishana madaraka kwa njia ya amani.

Lakini ikiwa matokeo ya uchaguzi huo yataleta mzozo, hali ya usalama inaweza kuzorota haraka, hususan katika eneo la Mashariki kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako kuna makundi kadhaa ya wanamgambo wanaobeba silaha.

Uchunguzi wa maoni kuelekea siku ya uchaguzi ulikuwa ukionyesha wagombea wa upinzani Martin Fayulu na Felix Tsishekedi wakiongoza na kumwacha nyuma Emmanuel Ramazani Shadary anayegombea kwa tiketi ya muungano tawala na kuungwa mkono na rais Kabila.../