Jeshi la Kenya laua magaidi 7 wa al-Shabaab Somalia
(last modified Wed, 02 Jan 2019 07:22:49 GMT )
Jan 02, 2019 07:22 UTC
  • Jeshi la Kenya laua magaidi 7 wa al-Shabaab Somalia

Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limetangaza kufanikiwa kuwaangamiza magaidi saba wa kundi la al-Shabaab na kuwajeruhi wengine kadhaa katika operesheni ya kusini mwa Somalia.

Katika taarifa yake, KDF imesema imefanikiwa kukamata bunduki 9 aina ya AK 47 na zana mbili za kurusha makombora katika oparesheni iliyofanyika Januari Mosi saa tano asubuhi.

Taarifa hiyo imesema mapigano hayo yamejiri katika barabara ya Tabda-Delahola ambapo kulijiri mapigano makali baina ya wanajeshi wa Kenya na magaidi wakufurishaji wa Al-Shabaab. Msemaji wa KDF PM Njuguna amesema askari wa jeshi hilo wataendelea kuwa macho na kuwasaka magaidi ili kuhakikisha amani inadumu nchini Kenya na pia kwa lengo la kuunga mkono oparesheni za Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika, AMISOM, nchini Somalia ili uthabiti urejee katika nchi hiyo jirani.

Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya ndani kwa robo karne sasa.

Tags