SADC yaubariki uchaguzi wa Kongo DR licha ya ghasia na malalamiko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50596-sadc_yaubariki_uchaguzi_wa_kongo_dr_licha_ya_ghasia_na_malalamiko
Huku zoezi la kuhesabu kura likiendelea katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imesema uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita nchini humo ulifanyika vizuri kwa kiasi kikubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2019 23:42 UTC
  • SADC yaubariki uchaguzi wa Kongo DR licha ya ghasia na malalamiko

Huku zoezi la kuhesabu kura likiendelea katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imesema uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita nchini humo ulifanyika vizuri kwa kiasi kikubwa.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na SADC imesema zoezi hilo lilifanyika katika mazingira huru na limeenda vizuri kwa kiasi kikubwa, licha ya kushuhudiwa ghasia za hapa na pale zilizofanya idadi kubwa ya watu kutopiga kura katika baadhi ya maeneo.

Taarifa ya  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika imetolewa katika hali ambayo, wagombea wakuu wa upinzani katika uchaguzi huo wamedai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi, ikiwemo kukwama kwa mashine za kupigia kura za BVR.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI aidha iliakhirisha uchaguzi katika maeneo matatu ya nchi hiyo ya Beni, Butembo na Yumbi kutokana na ugonjwa wa Ebola na mapigano ya kikabila hadi mwezi Machi mwaka huu, hatua ambayo iliwanyima fursa wapiga kura zaidi ya milioni moja kushiriki uchaguzi huo.

Zoezi la kuhesabu kura DRC

Wagombea watatu wanaochuana vikali kuwania kiti cha urais ni Emmanuel Ramadhan Shadary wa chama tawala FCC anayeungwa mkono na rais anayeondoka, Joseph Kabila, Martin Fayulu wa muungano wa upinzani wa Lamuka na Felix Tshisekedi wa chama cha UDPS.

CENI imesema mshindi wa uchaguzi wa rais atatangazwa kufikia tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari, 2019.