CENI: Matokeo ya muda ya uchaguzi wa DRC huenda yakacheleweshwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI imesema yumkini italazimika kuchelewesha matokeo ya muda ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili iliyopita kutokana na sababu za kiufundi.
Mwenyekiti wa CENI, Corneille Nangaa hii leo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Tunafanya juu chini ili kuhakikisha kuwa matokeo haya yanachapishwa kufikia Januari 6 (Jumapili ijayo), lakini ikishindikana hatutakuwa na budi kuchelewa kutoa matokeo hayo."
CENI imesema mshindi wa uchaguzi wa rais atatangazwa rasmi kufikia tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari, 2019.
Hii ni katika hali ambayo, wagombea wakuu wa upinzani katika uchaguzi huo wamedai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi, ikiwemo kukwama kwa mashine za kupigia kura za BVR. Aidha ghasia za hapa na pale zilishuhudiwa na kufanya idadi kubwa ya watu kutopiga kura katika baadhi ya maeneo.
Vyama vya upinzani vinadai kuwa karatasi za kupigia kura za wagombea wao zimetapakaa katika baadhi ya maeneo hususan kwenye ngome zao za kisiasa, na hivyo baadhi ya vyama hivyo vimesema havina imani na mchakato wa kuhesabu kura.
Hata hivyo timu za waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimesema uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita nchini humo ulifanyika vizuri kwa kiasi kikubwa.