Hali ya wasiwasi yatanda DRC kabla ya matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50664-hali_ya_wasiwasi_yatanda_drc_kabla_ya_matokeo_ya_uchaguzi
Hali imeripotiwa kuwa tete katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumamosi hii, ikiwa yamesalia masaa machache kabla ya kutangazwa matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2019 12:02 UTC
  • Hali ya wasiwasi yatanda DRC kabla ya matokeo ya uchaguzi

Hali imeripotiwa kuwa tete katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumamosi hii, ikiwa yamesalia masaa machache kabla ya kutangazwa matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.

Licha ya kuwa Tume ya Uchaguzi DRC, CENI, ilikuwa imetangaza kuwa matokeo ya mwisho yatatangawa kesho Januari 6, wakuu wa tume hiyo wameonya kuwa yamkini kukawa na ucheleweshaji wa tangazo la matokeo ya awali, hatua ambayo huenda ikaibua mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.

Mnamo Disemba 30, wagombea 21 walipigiwa kura katika mchuano wa nani atachukua nafasi Rais Joseph Kabila ambaye ameitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 18 sasa. Wagombea watatu wanaochuana vikali kuwania kiti cha urais ni Ramadhan Shadary wa chama tawala FCC, Martin Fayulu wa Lamuka na Felix Tchisekedi wa UDPS.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jana Ijumaa lilikutana katika kikao cha faragha kujadili uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkutano huo uliombwa kufanyika na nchi ya Ufaransa wakati huu Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wakizitaka mamlaka nchini humo kuheshimu matokeo ya uchaguzi uliofanyika Disemba 30.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuendelea kukamatwa kwa wanasiasa na raia kutoka katika vituo vya kuhesabia kura. Umoja huo umesema vitendo vya ukamataji havikubaliki na unafuatilia kwa karibu yanayojiri.

Tayari waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamesema uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita nchini humo ulifanyika vizuri kwa kiasi kikubwa.