Uchaguzi DRC; CENI yatetea uamuzi wa kuakhirisha matokeo ya muda
Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imetetea uamuzi wake wa kuchelewesha matokeo ya muda ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita, ikisisitiza kuwa kufikia sasa haijaweza kuhesabu hata nusu ya kura zilizopigwa.
Matokeo hayo ya awali yalitazamiwa kutangazwa leo Jumapili. Hata hivyo maafisa wa CENI jana walisema kufikia sasa wameweza kuhesabu asilimia 47 tu ya kura hizo.
Hali kadhalika wameahidi kuwa matokeo hayo ya muda yatatangazwa wiki ijayo.
Siku ya Ijumaa, Mwenyekiti wa CENI, Corneille Nangaa alisema huenda matokeo hayo ya muda ya uchaguzi wa rais yakacheleweshwa kutokana na sababu za kiufundi.
CENI imesema mshindi wa uchaguzi wa rais atatangazwa rasmi kufikia tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari, 2019.
Wagombea watatu wanaochuana vikali kuwania kiti cha urais ni Ramadhan Shadary wa chama tawala FCC, Martin Fayulu wa Lamuka na Felix Tchisekedi wa UDPS.