Watu 8 wauawa katika shambulizi mashariki mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50730-watu_8_wauawa_katika_shambulizi_mashariki_mwa_kongo_dr
Kwa akali raia wanane wameuawa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kijiji kimoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2019 11:09 UTC
  • Watu 8 wauawa katika shambulizi mashariki mwa Kongo DR

Kwa akali raia wanane wameuawa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kijiji kimoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mak Hazukay, msemaji wa jeshi katika eneo la Beni, mashariki mwa DRC amesema hujuma hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia leo, katika kijiji cha Mavivi.

Amesema raia wanane, wakiwemo watu wanne wa familia za wanajeshi wa serikali katika eneo hilo wameuawa katika shambulio hilo. 

Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa pia katika shambulio hilo la watu waliojizatiti kwa silaha. Hata hivyo utambulisho wa wavamizi hao haujaweza kubainika mara moja.

Hii ni katika hali ambayo, polisi katika kijiji hicho inasema idadi ya waliouawa katika hujuma hiyo ni raia kumi.

Wanamgambo wa ADF, mashariki mwa DRC

Ifahamike kuwa, kundi la wanamgambo wa ADF ndilo limekuwa likitekeleza aghalabu ya mashambulizi na mauaji ya kuvizia katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwezi uliopita wa Disemba, wapiganaji hao wa ADF wa Uganda waliuawa raia 17 katika eneo la Mangolikene, nje kidogo ya mji wa Beni, eneo la Kivu Kaskazini.