Afrika Kusini, Zambia zaitaka Tume ya Uchaguzi Kongo itangaze matokeo ya urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50756-afrika_kusini_zambia_zaitaka_tume_ya_uchaguzi_kongo_itangaze_matokeo_ya_urais
Marais wa Afrika Kusini na Zambia wameitaka tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais ili kuondoa taharuki na wasiwasi wa kuibuka ghasia za baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2019 13:31 UTC
  • Afrika Kusini, Zambia zaitaka Tume ya Uchaguzi Kongo itangaze matokeo ya urais

Marais wa Afrika Kusini na Zambia wameitaka tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais ili kuondoa taharuki na wasiwasi wa kuibuka ghasia za baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Cyril Ramaphosa na Edgar Lungu wametoa mwito huo leo Jumatano nchini Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, kutolewa matokeo hayo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiko kutakorejesha hali ya utulivu na uthabiti katika nchi hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa, Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa (CENI) jana Jumanne alisema tume hiyo itatangaza matokeo ya muda kati ya masaa 24 hadi 48 yajayo.

Huku matokeo hayo yakisuburiwa kutangazwa wakati wowote kutoka sasa, askari polisi wa kukabiliana na fujo wametapakaa katika kila pembe ya makao makuu ya CENI mjini Kinshasa.  

Mwenyekiti wa CENI, Corneil Nangaa

Wagombea watatu wanaochuana vikali kuwania kiti cha urais ni Ramadhan Shadary wa chama tawala FCC, Felix Tshisekedi wa UDPS na Martin Fayulu wa muungano wa upinzani wa Lamuka ambaye chunguzi za maoni za kabla ya uchaguzi  zilionyesha kuwa yuko katika nafasi kubwa ya kuibuka mshindi.

CENI imesema mshindi wa uchaguzi huo wa rais uliofanyika Disemba 30 mwaka uliomalizika atatangazwa rasmi kufikia tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari.