António Guterres: Wakongomani wajiepushe na machafuko katika kipindi hiki nyeti
Kufuatia kutolewa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amezitaka pande mbalimbali kujiepusha na vitendo vya utumiaji mabavu.
Guterres ameyasema hayo Alkhamisi ya leo ambapo amezitaka pande husika nchini humo kutatua tofauti za uchaguzi kupitia msaada wa katiba na pia sheria za uchaguzi. Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI, imemtangaza Felix Tshisekedi, wa kambi ya upinzani kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 30 Disemba mwaka jana. Matokeo ya tume hiyo ya uchaguzi yanatofautiana na matokeo ya Kamisheni ya Taifa ya Maaskofu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa kamisheni hiyo, Martin Fayulu wa kambi nyingine ya upinzani ndiye mshindi wa uchaguzi huo.
Aidha habari zaidi zinaarifu kwamba maafisa usalama wameweka doria maeneo yote ya karibu ya Tume ya Uchaguzi CENI na kadhalika Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo kwa lengo la kuzuia ghasia zozote zinazoweza kutokea. Uchaguzi mkuu wa rais nchini humo ulifanyika Jumapili ya tarehe 30 mwezi uliopita wa Disemba 2018, katika hali ambayo nchi hiyo hadi sasa bado inakabiliwa na machafuko na maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila. Iwapo matokeo hayo yataidhinishwa, Felix Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza wa upinzani kushinda uchaguzi wa rais tangu Kongo ipate uhuru wake miaka 59 iliyopita.