Uchaguzi wa Kongo DR na kuendelea mivutano ya kisiasa
-
Rais mteule wa DRC, Felix Tchisekedi
Siku ya Alkhamisi Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) ilimtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa kiti cha urais baada ya kujinyakulia asilimia 38.57 ya kura.
Hata hivyo tangazo hilo lilipokelewa kwa hisia mseto na radiamali mbalimbali huku mvutano wa kisiasa ukiibuka na kushika kasi. Watu wasiopungua 11 wanaripotiwa kuuawa kufuatia machafuko yaliyozuka baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais na makumi ya wengine wamejeruhiwa. Uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulifanyika katika hali ambayo, nchi hiyo kwa miezi kadhaa ilishuhudia mivutano mingi ya kisiasa. Kubakia madarakani Rais Joseph Kabila hata baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi kwa mujibu wa Katiba na kuakhirishwa zoezi la uchaguzi kwa mara kadhaa ni mambo ambayo yaliwakasirisha mno wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Licha ya uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kucheleweshwa na kuakhirishwa mara kadhaa, lakini hatimaye ulifanyika tarehe 30 Disemba mwaka jana. Ushindani mkubwa katika uchaguzi wa Rais ulikuwa baina ya wagombea watatu ambao ni Emmanuel Ramazani Shadary aliyegombea kwa tiketi ya muungano unaotawala, Felix Tshisekedi aliyegombea kwa tiketi ya chama chake cha UDPS na kile cha UNC cha Vital Kamerhe na Martin Fayulu wa muungano wa Lamuka. Felix Tshisekedi alitangazwa mshindi wa kiti cha Urais katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni ulikuwa ukionyesha kwamba, Martin Fayulu ndiye ambaye angepata ushindi na hata ushindi wa Tshisekedi umewashangaza wengi.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuna uwezekano kumefanyika udanganyifu katika uchaguzi huo na akthari yao wanasema kuwa, kutangazwa Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo, ni matokeo ya mazungumzo ya siri yaliyofanyika baina ya serikali ya Kinshasa na Tshisekedi kwa ajili ya maridhiano na kugawana madaraka. Filhaal, wafuasi wa Tshisekedi wanaamini kwamba, ushindi wa mgombea wao ni mwanzo wa duru mpya ya uongozi nchini humo,. Hata hivyo, kundi la watu wengine akiwemo Martin Fayulu, wagombea wengine pamoja na Kanisa Katoliki wametangaza kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Kuhusiana na hilo, siku ya Alkhamisi Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alizitaka pande zote katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutatua hitilafu za uchaguzi kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi hiyo.
Endapo ushindi wa Felix Tshisekedi utathibitishwa na Mahakama ya Katiba katika kipindi cha siku kumi, mwanasiasa huyo atakuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya uchaguzi huru na wa demokrasia tangu zama za Patrice Lumumba mwanasiasa na Waziri Mkuu wa kwanza wa Congo. Rais Joseph Kabila amekuwa madarakani tangu mwaka 2011 baada ya kuuawa baba yake yaani Laurent-Désiré Kabila. Katika kampeni zake za uchaguzi, Felix Tshisekedi aliahidi kurejesha amani nchini humo, kupambana na ufisadi, kuondoa umasikini na kuboresha mazingira ya uchumi.
Ahadi hizo zilitolewa katika hali ambayo, kwa miaka mingi sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama, machafuko ya ndani hususan katika maeneo ya mpakani. Katika upande mwingine, Congo DR inakabiliwa na ufisadi mkubwa, uingiliaji wa madola ya magharibi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo hususan Ufaransa na kuenea maradhi ya Ebola. Haya ni baadhi ya mambo ambayo yameshadidisha matatizo ya wananchi wa nchi hiyo.
Kushadidi sokomoko na mivutano ya kisiasa, kukosekana uhuru wa kisiasa na kiraia na ukandamizaji dhidi ya wapinzani ni matatizo mengine yanayowakabili wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Katika hali ambayo, wachambuzi wa mambo walikuwa na matumaini ya kufanyika ubadilishanaji madaraka kwa njia ya amani, lakini filihali kwa kuzingatia anga ya kisiasa inayotawala nchini humo, si jambo lililo mbali katika siku za usoni kukashuhudiwa kuongezeka mivutano na malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.