UN yapinga madai ya Morocco kuhusu Polisario
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50854-un_yapinga_madai_ya_morocco_kuhusu_polisario
Umoja wa Mataifa umepinga madai ya Morocco ya kwamba Harakati ya Polisario ya ukombozi wa Sahara Magharibi imevunja makubaliano ya kusimamisha vita na kusisitiza kuwa, hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa Polisario imevunja makubaliano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2019 03:46 UTC
  • UN yapinga madai ya Morocco kuhusu Polisario

Umoja wa Mataifa umepinga madai ya Morocco ya kwamba Harakati ya Polisario ya ukombozi wa Sahara Magharibi imevunja makubaliano ya kusimamisha vita na kusisitiza kuwa, hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa Polisario imevunja makubaliano hayo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo mapema leo asubuhi na kuunukuu Umoja wa Mataifa ukijibu barua mbili za malalamiko zilizowasilishwa kwake na Morocco zinazodai kuwa harakati ya Polisario imevunja makubaliano ya kusimamisha vita katika eneo la Ha'il huko Sahara Magharibi na kusisitiza kuwa, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa walioko Sahara Magharibi hawajaona uvunjaji wowote wa makubaliano ya kusitisha vita katika eneo hilo.

Stéphane Dujarric, msemaji rasmi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amewaambia waandishi wa habari mjini New York Marekani kwamba wawakilishi wa umoja huo huripoti haraka sana uvunjaji wowote wa makubaliano ya usitishaji vita katika eneo hilo, lakini kuhusu suala hili linalodaiwa na Morocco, hakuna ripoti yoyote kutoka kwa wawakilishi hao.

Stéphane Dujarric

Dujarric pia amesema, Umoja wa Mataifa umekuwa makini sana katika kusimamia makubaliano ya kusimamishwa vita katika eneo la Sahara Magharibi tangu pande mbili hasimu zilipotiliana saini makubaliano hayo.

Mgogoro wa Sahara Magharibi ulianza mwaka 1975 baada ya kufurushwa wakoloni wa Uhispania katika eneo hilo. Morocco ililiteka eneo hilo, lakini harakati ya Polisario ambayo iliundwa mwaka 1973 ili kupambana na wakoloni wa Uhispania inasema kuwa Sahara Magharibi ni nchi huru inayokaliwa kwa mabavu na Morocco.