Jan 15, 2019 15:30 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika shambulizi la kigaidi Nairobi, Kenya

Kwa akali watu watatu wamethibitishwa kuuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi, lililotokea katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Vyombo vya habari nchini humo vimesema magaidi wamevamia Hoteli ya Dusit katika mtaa wa Westland jijini Nairobi, na kuanza kufyatua risasi ovyo. 

Mashuhuda wanasema walisikia sauti kubwa ya mripuko kabla ya milio ya risasi kuanza kurindima kwenye jengo hilo.

Mkuu wa Polisi nchini humo, Inspekta Jenerali Joseph Boinnet amethibitisha kutokea shambulizi hilo, ingawaje hajaeleza idadi ya wahanga.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia limetangaza kupitia radio yake ya kipropaganda ya Andalus kuwa limehusika na shambulizi hilo.

Jengo la Westgate lililoshambuliwa na al-Shabaab 2013

Msemaji wa genge hilo la ukufurishaji, Abdiasis Abu Musab amesema "Sisi ndio tumehusika na shambulizi la Nairobi. Operesheni inaendelea. Tutatoa maelezo zaidi baadaye."

Shambulizi hilo limetokea mita chache kutoka Jengo la Westgate ambalo lilishambuliwa na wanachama wa al-Shabaab mwaka 2013, ambapo watu 67 waliuawa.

Tags