Ethiopia yawakamata wapiganaji 800 wa Oromia wakiwa na silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50954-ethiopia_yawakamata_wapiganaji_800_wa_oromia_wakiwa_na_silaha
Serikali ya Ethiopia imesema katika wiki za hivi karibuni imewakamata waasi 835 wenye silaha wakati hali ya wasiwasi ikiendelea kuongezeka kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo la Oromia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 18, 2019 04:51 UTC
  • Ethiopia yawakamata wapiganaji 800 wa Oromia wakiwa na silaha

Serikali ya Ethiopia imesema katika wiki za hivi karibuni imewakamata waasi 835 wenye silaha wakati hali ya wasiwasi ikiendelea kuongezeka kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo la Oromia.

Kituo cha uongozi kilichoanzishwa na serikali ya Ethiopia kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye majimbo ya Oromia na Benishagul Gumuz, kimesema waasi waliokamatwa ni wapiganaji wa kundi la Oromo Liberation Front. Kituo hicho pia kimekanusha uvumi kuwa jeshi la anga la nchi hiyo limefanya mashambulizi kwenye jimbo la Oromo.

Taarifa ilitolewa na kituo hicho baada ya ripoti zinazotolewa na wanaharakati na vyombo vya habari vya nje, kuwa jeshi la anga la Ethiopia lilifanya mashambulizi dhidi ya vituo vya kundi la Oromo Liberation Front. Kamanda wa jeshi la anga la Ethiopia Brigedia Jenerali Yilma Merdasa amesema ripoti hizo si za kweli na zina nia mbaya ya kuvuruga amani na usalama.

Machafuko katika eneo la Oromia yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

 Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia

Wakaazi wa eneo hilo wanailaumu serikali ya Addis Ababa wakidai kuwa ndiyo iliyowasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao kama ambavyo walilalamikia pia ukandamizaji wa kisiasa wanaofanyiwa na serikali hiyo.

Wakosoaji wa Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa nchi hiyo wanaamini kwamba marekebisho ya kisiasa aliyoyafanya ndiyo yameibua tena mapigano ya kikabila nchini humo. Mapigano ya kikabila ya mwaka jana nchini Ethiopia yalipelekea karibu watu milioni tatu kuwa wakimbizi. Mapigano ya mwisho ya kikabila ni yale yaliyoshuhudiwa kati ya watu wa kabila la Afars na Issa Somalia ambazo ni jamii za wachache katika eneo hilo na ambayo yalitokea mwezi Disemba uliopita. Katika mapigano hayo makumi ya watu waliuawa.