Ethiopia yawaachia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa
Serikali ya Ethiopia imewaachia huru wafungwa wa kisiasa zaidi ya 13 elfu katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Shirika la habari la serikali la FANA limetangaza kuwa, wafungwa hao wameachiwa huru katika fremu ya marekebisho ya haraka ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanashuhudiwa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika tokea Waziri Mkuu, Abiy Ahmed aingie madarakani mwezi Aprili mwaka jana.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu nchini humo imesema imewapa cheti cha kuachiwa huru wafungwa 13,200 kufikia sasa, ambapo aghalabu yao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za uhaini na ugaidi.
Miezi michache iliyopita serikali ya Ethiopia iliendeleza wimbi la kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, ambapo iliwaondoa gerezani wafungwa 2,345 waliotuhumiwa kuhusika na machafuko yaliyolikumba eneo la Oromiya kati ya 2015 na 2016.
Serikali iliyotangulia ya Hailemariam Desalegn iliwakamata na kuwafunga jela karibu watu 30,000 kwa tuhuma za ugaidi kama njia ya kukabiliana na maandamano.
Kati ya waliofungwa jela walikuwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, viongozi wa upinzani, waandishi habari na wanablogu.