Mahakama Nigeria yataka jopo lisikize kesi dhidi ya Jaji Mkuu aliyesimamishwa kazi
Mahakama ya Rufaa nchini Nigeria hii leo imetoa uamuzi wa kutaka jopo la uchunguzi lisikilize kesi inayomuandama Jaji Mkuu wa nchi hiyo aliyesimamishwa kazi hivi karibuni.
Mahakama hiyo imesema kesi ya Jaji huyo, Walter Onnoghen ambaye alisimamishwa kazi na Rais Muhammadu Buhari wiki iliyopita kwa tuhuma za kukiuka sheria inayowataka watumishi wa umma kutangaza mali na utajiri wao, inaweza kusikilizwa na Jopo la Maadili ya Kazi.
Mkuu cha chama cha upinzani cha Peoples Democratic Party (PDP), Atiku Abubakar aliuataja uamuzi huo wa Ijumaa iliyopita kama udikteta wa kupindukia, akisisitiza kuwa huo ni mwendelezo wa ubakaji wa demokrasia iliyopiganiwa kwa jitihada kubwa nchini.
Wakuu wa chama hicho cha PDP wametilia shaka uamuzi huo wa Buhari wa kumsimamisha kazi Walter Onnoghen, siku chache kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi ujao wa Februari.
Jaji Mkuu nchini Nigeria ni Rais wa Mahakama ya Juu yenye jukumu la kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa matokeo ya urais.
Ingawa kuna wagombea zaidi ya 70 ambao wamejitokeza kuwania kiti cha urais nchini Nigeria lakini ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya Rais wa sasa Muhamadu Buhari na mgombea wa chama kikuu cha upinzani PDP Atiku Abubakar aliyewahi kuwa Makamu wa Rais.