Mkutano wa kujadili mchakato wa uchaguzi wa Libya huenda ukacheleweshwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51247-mkutano_wa_kujadili_mchakato_wa_uchaguzi_wa_libya_huenda_ukacheleweshwa
Umoja wa Mataifa huenda ukasogeza mbele tarehe ya mkutano wa kuratibu uchaguzu mkuu wa Libya uliopangwa kufanyika mwaka huu hadi viongozi wa mirengo hasimu ya nchi hiyo watakapotoa msukumo na uungaji mkono zaidi kwa mchakato huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 31, 2019 23:13 UTC
  • Mkutano wa kujadili mchakato wa uchaguzi wa Libya huenda ukacheleweshwa

Umoja wa Mataifa huenda ukasogeza mbele tarehe ya mkutano wa kuratibu uchaguzu mkuu wa Libya uliopangwa kufanyika mwaka huu hadi viongozi wa mirengo hasimu ya nchi hiyo watakapotoa msukumo na uungaji mkono zaidi kwa mchakato huo.

Hayo yameelezwa na duru zilizo karibu na waandaaji wa mkutano huo.

Mkutano wa kitaifa ndio nukta kuu ya ramani ya njia iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na madola ya Magharibi kwa ajili ya uchaguzi, unaolenga kuinasua Libya kwenye mkwamo wa vita vya miaka minane tangu ulipoangushwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Kucheleweshwa kwa mkutano huo unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, utakaotoa fursa kwa Walibya wa matabaka yote kuamua kama wawe na mfumo wa utawala wa urais au bunge, utasababisha kusogezwa mbele pia tarehe ya kufanyika uchaguzi wenyewe.

Awali uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika Desemba 10 mwaka uliomalizika wa 2018 lakini zoezi hilo liliahirishwa kutokana mpasuko uliojitokeza baina ya viongozi wa mirengo hasimu na wimbi la mapigano na machafuko yaliyozuka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Ghassan Salame

Kufuatia mkwamo huo, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame alitaka mkutano wa uchaguzi ufanyike katika "wiki za mwanzo za mwaka 2019" na uchaguzi wenyewe ufanyike mwezi Juni mwaka huu. Hata hivyo duru zilizo karibu na mpango huo wa Umoja wa Mataifa zimeeleza kuwa Salame hatotangaza tarehe na mahali utakapofanyika mkutano huo hadi atakapopata uungaji mkono wa kutosha kutoka pande zote husika nchini Libya. Taarifa zaidi zinasema huenda mkutano huo ukasogezwa mbele hadi mwezi Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia, mkutano wa uchaguzi ndiyo "turufu ya mwisho" ya mjumbe huyo maalumu wa UN ambaye amekuwa akitoa msukumo kwa suala hilo tangu mwezi Septemba 2017. 

Libya haijawahi kuwa na utulivu na amani ya hata siku moja tangu mwaka 2011 baada ya Marekani kuongoza jeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kusambaratisha miundombinu yake yote pamoja na kuacha silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi hasimu, ambayo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi hivi sasa nchini humo.../