IGAD yasikitishwa na ukiukwaji mapatano ya amani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51262-igad_yasikitishwa_na_ukiukwaji_mapatano_ya_amani_sudan_kusini
Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imebainisha masikitiko yake kuhusu ukiukaji wa mapatano ya amani yaliyosainiwa mwaka jana na pande hasimu nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2019 10:14 UTC
  • IGAD yasikitishwa na ukiukwaji mapatano ya amani Sudan Kusini

Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imebainisha masikitiko yake kuhusu ukiukaji wa mapatano ya amani yaliyosainiwa mwaka jana na pande hasimu nchini Sudan Kusini.

Mjumbe maalumu wa IGAD anayeshughulikia suala la Sudan Kusini Ismail Wais amesema baada ya kukumbwa  na vita kwa zaidi ya miaka mitano, watu wa Sudan Kusini sasa wanataraji kujenga upya maisha yao, na hivyo vitendo vya kukiuka mapatano ya amani havikubaliki.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Tume ya Kuchunguza Utekelezaji wa Makubaliano ya Amani Sudan Kusini RJMEC, serikali na makundi ya waasi wote wamehusika na vitendo vya ukiukaji mapatano ya amani hasa huko Yei.

Mapatano ya amani ya Sudan Kusini yalitiwa saini mwezi Septemba mwaka 2018, kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi, lakini yamekuwa yakikiukwa mara kadhaa .

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza tarehe 15 Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake wakati huo Riek Machar kwa madai kuwa alipanga njama ya kumpindua. Hadi hivi sasa watu laki tatu na 85 elfu wameshauawa na mamilioni ya wengine wamejeruhiwa na kuwa wakimbizi.

Sudan Kusini ilijitenga na ndugu zao wa Sudan mwaka 2011 na tangu wakati huo hadi sasa haijawahi kuwa na utulivu wa kudumu, bali imekuwa ikisumbuliwa na mizozo hii na ile.