Jeshi la Taifa Libya ladhibiti medani kubwa zaidi ya mafuta nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51498-jeshi_la_taifa_libya_ladhibiti_medani_kubwa_zaidi_ya_mafuta_nchini_humo
Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limedhibiti kikamilifu medani na kisima kikubwa zaidi cha mafuta cha nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2019 04:27 UTC
  • Jeshi la Taifa Libya ladhibiti medani kubwa zaidi ya mafuta nchini humo

Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limedhibiti kikamilifu medani na kisima kikubwa zaidi cha mafuta cha nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa, jeshi la Khalifa Haftar jana Jumatatu lilidhibiti kikamilifu kisima kikubwa na muhimu zaidi cha mafuta cha Libya cha el Sharara huko kusini mwa nchi hiyo baada ya kulizingira eneo hilo kwa siku kadhaa. 

Awali kisima hicho kilikuwa mikononi mwa serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na hadi sasa viongozi serikali hiyo hawajatoa tamko lolote kuhusiana na jambo hilo.

Wakati huo huo afisa mmoja wa Shirika la Mafuta la Libya ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa, vikosi vya jeshi la Khalifa Haftar vimetwaa kisima hicho cha mafuta bila ya mapigano na baada ya kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa kisima hicho. 

Libya

Kisima cha mafuta cha el Sharara ndicho kikubwa zaidi nchini Libya na kinazalisha mapipa laki tatu kwa siku ambayo ni sawa na thuluthi moja ya mafuta yote yanayozalishwa nchini humo. 

Libya imekuwa ikusumbuliwa na machafuko ya ndani tangu baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.