AU, UN kuandaa kongamano la maelewano Libya
Kamishna wa Amani na Usalama katika Umoja wa Afrika Smail Chergui amesema wameafikiana na Umoja wa Mataifa kuhusu kuandaa kongamano la maelewano ya kitaifa nchini Libya.
Akizungumza pembizoni mwa Mkutano wa 32 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia Chergui amesema kongamano hilo litakuwa jumuishi na litawaleta pamoja wadau wote nchini Libya.
Aidha amesema tarehe ya kufanyika uchaguzi Libya inaweza kutangazwa katika kongamano hilo. Chergui ametoa wito kwa nchi za kigeni kuacha kuingilia masuala ya Libya na kwamba watu wa Libya wameteswa kutokana na vita vya ndani na nchi za kigeni kuingilia masuala ya nchi yao.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.