Mustapha al-Khalfi: Hakuna mpango wa Benjamin Netanyahu kuitembelea Morocco
Serikali ya Morocco imekanusha taarifa za kuweko safari ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel katika nchi hiyo na kusema kuwa, habari hizo ni uvumi mtupu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mustapha al-Khalfi msemaji wa serikali ya Morocco amezipuuza taarifa za kuweko mpango wa Benjamin Netanyahu kuitembelea nchi hiyo na kusema kuwa serikali ya Rabat haitotoa majibu kwa uvumi.
Mustapha al-Khalfi amekadhabisha pia habari za kukutana na kufanya mazungumzo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Morocco na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel pambizoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York Marekakni Septemba mwaka jana.
Jumanne iliyopita, gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot liliripoti kwamba, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel atarajiwa kufanya safari nchini Morocco kabla yya kufanyika uchaguzi wa Bunge huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu Aprili mwaka huu.
Kuripotiwa taarifa za Benjamin Netanyahu kufanya safari nchini Morocco katika majuma machache yajayo kumekabiliwa na upinzani mkali ambapo hivi karibuni wanaharakati wa Morocco walifanya maandamano na kukusanyika mbele yya jengo la Bunge la nchi hiyo na kutangaza kuwa, hawataki Waziri Mkuu huyo wa utawala ghasibu wa Israel afanye safari katika nchi yao.
Harakati za kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu zimeongezeka zaidi baada ya Benjamin Netanyahu kufanya safari nchini Oman Oktoba mwaka jana, hatua ambayo ilipelekea Oman iandamwe kwa ukosoaji mkubwa.