Hofu ya Haftar kuuhujumu na kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52052-hofu_ya_haftar_kuuhujumu_na_kuuteka_mji_mkuu_wa_libya_tripoli
Wakaazi wa mji mkuu wa Libya, Tripoli wana hofu kubwa kuwa mji huo utahujumiwa na hatimaye kutekwa na askari kutoka eneo la mashariki mwa nchi hiyo wanaaongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 09, 2019 11:27 UTC
  • Hofu ya Haftar kuuhujumu na kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli

Wakaazi wa mji mkuu wa Libya, Tripoli wana hofu kubwa kuwa mji huo utahujumiwa na hatimaye kutekwa na askari kutoka eneo la mashariki mwa nchi hiyo wanaaongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.

Tayari askari wa Haftar wameteka eneo la kusini na kuchukua udhibiti wa visima vya mafuta katika eneo hilo.

Taarifa zinasema askari wa kundi linalojiita, Jeshi la Kitaifa la Libya linaloongozwa Haftar tayari wameshachukua udhibiti wa eneo la kati mwa nchi hiyo na wameonesha azma yao ya kuuteka mji mkuu, Tripoli.

Duru zinadokeza kuwa, Umoja wa Mataifa umeshtushwa na kasi ya kusonga mbele askari wanaoongozwa na Haftar. Kufuatia hali hiyo Umoja wa Mataifa umechukua hatua za dharura za kumpatanisha Khalifa Haftar anayetawala eneo la mashariki mwa Libya na serikali ya Libya inayotambuliwa na jamii ya kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Serraj.

Khalifa Haftar (kushoto) na Fayez al Serraj

Haftar, mwenye umri wa miaka 75, anaungwa mkono na Misri pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu na amesema haafikiani na serikali  ya al-Serraj.  Haftar amesisitiza kuwa askari wake watateka mji mkuu Tripoli jambo ambalo yamkini likaibua mapigano makubwa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.