Timu ya AU-UN iko Somalia kutathmini kazi kikosi cha kulinda amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52062-timu_ya_au_un_iko_somalia_kutathmini_kazi_kikosi_cha_kulinda_amani
Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) uko nchini Somalia kutathmini hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa Mpango wa Mpito wa Somalia ambao lengo lake kuu ni kuhamisha majukumu ya kulinda usalama kutoka Kikosi cha Askari wa Amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) na kuyakabidhi kwa Vikosi vya Kitaifa vya Usalama nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2019 21:48 UTC
  • Timu ya AU-UN iko Somalia kutathmini kazi kikosi cha kulinda amani

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) uko nchini Somalia kutathmini hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa Mpango wa Mpito wa Somalia ambao lengo lake kuu ni kuhamisha majukumu ya kulinda usalama kutoka Kikosi cha Askari wa Amani cha Umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) na kuyakabidhi kwa Vikosi vya Kitaifa vya Usalama nchini Somalia.

Ujumbe huo uko katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa lengo la kuchunguza hatua zilizochukuliwa na AMISOM katika kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika azimio nambari 2431 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia taarifa nambari 784 ya Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika.

Azimio la 2431 la Baraza la Usalama liliitaka AMISOM, ambayo ina askari karibu 21,000, ianze kupunguza askari 1000 mwezi uliopita wa Februari. Kiongozi wa ujumbe wa AU Meja Jenerali Okello amesema matokeo ya tathmini yao yatachangia maamuzi yatakayochukuliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika kuhusu kuongezwa muda wa kuhudumu askari wa AMISOM nchini Somalia.

Naye kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika kikao hicho cha Somalia Vincent Pasquini anasema watachunguza mpango wa mpito na maandalizi ya uchaguzi.

Askari wa AMISOM walipelekwa Somalia mwaka 2007 kuangamiza kundi la kigaidi la al Shabab na kuilinda serikali ya nchi hiyo.

Wanajeshi karibu 21,000 wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.