Rais Felix Tshisekedi wa DRC awaachia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa
Rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi amesaini dikrii ya kuwaachia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa.
Tshisekedi aliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais kuwa atawaachia huru wafungwa wa kisiasa waliorundikana katika magereza ya nchi hiyo, ndani ya siku 100 za uongozi wake.
Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais na Spika wa zamani wa Bunge la DRC, Vital Kamerhe amesema wafungwa 700 wa kisiasa wameachiwa huru katika hatua ya kwanza ya mpango huo wa serikali ya Tshisekedi, ambaye alishinda urais katika uchaguzi wa Disemba 30 mwaka jana.
Miongoni mwa viongozi mashuhuri wa upinzani walioachiwa huru katika msamaha huo wa Rais Tshisekedi ni Firmin Yangambi, Eugene Diomi Ndongala na Franck Diongo.
Aghlabu ya wafungwa wa kisiasa nchini humo walitiwa mbaroni baada ya kuendesha maandamano ya kupinga mabadiliko ya katiba yaliyokuwa na lengo la kuondoa ukomo wa muhula wa uongozi kwa rais hapo mwaka 2015.
Wanaharakati hao wa kisiasa walikamatwa kwa kile kilichotajwa na serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila kuwa ni makosa ya kufanya uasi, jinai za kivita na makosa ya kisiasa.