Amnesty International: Marekani inahusika katika kuwaua raia wa Somalia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa, jeshi la Marekani linahusika katika mauaji ya raia wa Somalia kupitia mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema kuwa, katika mashambulizi matano ya anga yaliyofanywa na jeshi la Marekani katika eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia, jumla ya raia 14 waliuawa na wengine wanane kujeruhiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi hayo yaliyotekelezwa kati ya Oktoba 2017 hadi Disemba mwaka jana, yalijiri wakati ambao Rais Donald Trump wa Marekani alibatilisha sheria ya ukomo wa matumizi ya nguvu za anga nchini Somalia.
Aidha ripoti hiyo imeongeza kwamba, mwaka jana pekee jeshi la Marekani lilitekeleza kwa akali mashambulizi 47 ya anga, huku mwaka mmoja kabla yaani 2017 likiwa limetekeleza mashambulizi 35 na mwaka 2016 likitekeleza zaidi ya hujuma 15 ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Somalia ilitumbukia katika vita vya ndani tangu mwaka 1991 baada ya kupinduliwa utawala wa kidikteta wa nchi hiyo wa Rais Mohamed Siad Barre. Vita na machafuko nchini Somalia vinajiri katika hali ambayo Marekani ina askari wake wanaokadiriwa kufikia 500 au 600 ndani ya nchi hiyo.