Wanajeshi wa Somalia wagoma kwa kutolipwa mishahara ya miezi minne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52307-wanajeshi_wa_somalia_wagoma_kwa_kutolipwa_mishahara_ya_miezi_minne
Azma ya Somalia ya kusimamia usalama wake pasi na kutegemea uungaji mkono wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (Amisom) imekumbwa na kizingiti, baada ya baadhi ya askari wa Somalia kufanya mgomo kulalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2019 11:24 UTC
  • Wanajeshi wa Somalia wagoma kwa kutolipwa mishahara ya miezi minne

Azma ya Somalia ya kusimamia usalama wake pasi na kutegemea uungaji mkono wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (Amisom) imekumbwa na kizingiti, baada ya baadhi ya askari wa Somalia kufanya mgomo kulalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa sasa.

Wakazi na wanajeshi wa Somalia wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, askari wa Somalia katika kambi tatu za kijeshi zilizoko katika eneo lenye ukosefu wa usalama la Shabelle wanafanya mgomo kushinikiza kulipwa mishahara yao ya miezi minne.

Mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Ulinzi la Somalia SDF Kanali Abdi Mohamed Ahmed amenukuliwa na Reuters akisema kuwa, "Kambi ambazo askari wa Somalia wamezigura ziko Shabelle ya Kati, na hatua hiyo imesababishwa na wao kutolipwa mishahara yao kwa muda wa miezi minne. Hivi sasa tuko njiani tunaelekea Mogadishu. Inauma sana kusimama kidete kupambana na al-Shabaab ilhali mke na watoto wako wanalala na njaa."

Hii ni katika hali ambayo, Hassan Ali Kheire, Waziri Mkuu wa Somalia Jumanne iliyopita alisema kuwa, askari wa serikali ya Somalia ambao hawajalipwa mishahara yao ni wale tu ambao hawajasajiliwa na kwamba majina yao yakishasajiliwa watalipwa.

Askari wa Amisom wanaoshirikiana na wanajeshi wa Somalia kupambana na al-Shabaab

Wanajeshi hao wa Somalia wamekuwa wakishirikiana na askari karibu 21,000 wa Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, kuangamiza kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na kuilinda serikali ya nchi hiyo tokea mwaka 2007.

Serikali dhaifu ya Mogadishu imekuwa ikitegemea taasisi na nchi wafadhili katika mahitaji yake mbalimbali.