Wapinzani nchini Misri wakosoa azma ya kuondoa kikomo cha urais
(last modified Thu, 28 Mar 2019 04:45:42 GMT )
Mar 28, 2019 04:45 UTC
  • Wapinzani nchini Misri wakosoa azma ya kuondoa kikomo cha urais

Muungano wa upinzani nchini Misri umekosoa vikali mpango wa kuondoa kikomo cha muhula wa rais, hatua ambayo huenda ikamruhusu Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo kugombea zaidi ya mihula miwili iliyoruhusiwa na katiba.

Katika kikao na waandishi wa habari Jumatano mjini Cairo, muungano huo wa Civil Democratic Movement unaovijumuisha vyama kadhaa vya upinzani kupitia msemaji wake, Magdi Abdel-Hamid umesema kuwa, marekebisho hayo ya katiba yatavunja misingi ya uhuru, dekomkrasia na uwepo wa utawala wa kiraia.

Muungano huo umesema iwapo marekebisho hayo ya katiba yatapasishwa na kutekelezwa, itakuwa ndo kwanza milango ya udikteta na ubabe imefunguliwa.

Mwezi uliopita, Bunge la Misri lilipasisha hoja inayoruhusu kukifanyia marekebisho kipengee cha 140 cha katiba, ambacho kinasema rais anapaswa kugombea mihula miwili pekee ya miaka minne minne.

Rais wa Misri

Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo wananchi wa Misri watapewa fursa ya kushiriki kura maoni ya ima kuyaunga mkono au kuyapinga marekebisho hayo ya katiba, ambayo yakipasishwa huenda Sisi akabakia madarakani hadi mwaka 2034.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya al-Sisi imekuwa ikikosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani na hasa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin sambamba na kuviwekea mbinyo vyombo vya habari, tangu kiongozi ashike hatamu za uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013.

Tags