Sudan Kusini yaandaa mkutano wa kuwavutia wawekezaji baada ya vita kumalizika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52491-sudan_kusini_yaandaa_mkutano_wa_kuwavutia_wawekezaji_baada_ya_vita_kumalizika
Sudan Kusini imeandaa mkutano wa uwekezaji, ukiwa ni wa kwanza kufanyika baada ya kumalizika rasmi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, viliyodumu kwa miaka mitano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2019 21:48 UTC
  • Sudan Kusini yaandaa mkutano wa kuwavutia  wawekezaji baada ya vita kumalizika

Sudan Kusini imeandaa mkutano wa uwekezaji, ukiwa ni wa kwanza kufanyika baada ya kumalizika rasmi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, viliyodumu kwa miaka mitano.

Mratibu wa mkutano huo Akol Nyok amesema, mkutano huo unaoitwa "Kufanya Biashara nchini Sudan Kusini" unalenga kuunganisha mashirika ya kimataifa, watu binafsi na mashirika binafsi na fursa za uwekezaji za nchi hiyo.

Mkutano huo wa siku moja ambao ulifanyika jana Ijumaa umewezesha maofisa wa serikali na wawekezaji wa ndani na nje kushiriki katika maonesho, vikao vya mawasiliano na majadiliano ya vikundi mbalimbali.

Nyok pia amesema, kuna haja ya kuwasilisha habari kati ya watu wanaofanya biashara nchini humo na watu kutoka nje, huku akiongeza kuwa mkutano huo unaweza kuwa chombo cha kutoa habari halisi kwa watu wanaofanya biashara katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Sudan Kusini, ndio nchi inayotegemea zaidi pato la uuzaji mafuta ya petroli duniani ambapo pato hilo la mafuta ni asilimia 60 ya Pato Ghafi la Ndani (GDP) la nchi hiyo.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba mwaka 2013 na hivyo uzalishaji mafuta ukapungua kutoka mapipa 350,000 kwa siku mwaka 2011, hadi chini ya 130,000 mwaka 2014 na hivyo kuvuruga kabisa uchumi wa nchi hiyo. Aidha nchi hiyo ina uwezo mkubwa wa kilimo ambao bado haujatumiwa. Inakadiriwa kuwa ni asilimia 4 tu ya ardhi ya kilimo ya Sudan Kusini ndiyo inayotumika hivi sasa.  Nchi hiyo pia inakadiriwa kuwa na mifugo ipatayo milioni 30 wakiwamo ng'ombe, mbuzi na kondoo. Kizingiti kikubwa cha uwekezaji Sudan Kusini kimetajwa kuwa hofu ya wawekezaji, kama pande hasimu zitaendelea kutekeleza mapatano ya amani ya Septemba 2018 au la.