Buhari: Libya ni tishio kwa usalama wa Afrika
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametahadharisha kwamba Libya inaweza kuwa tishio kwa bara zima la Afrika.
Rais wa Nigeria amesema hali ya kusini mwa Libya haidhibitiki na kwamba eneo hilo limekuwa soko kubwa la silaha, suala ambalo amesisitiza kuwa linahatarisha usalama wa Nigeria na nchi nyingine za Afrika.
Buhari amesisitiza kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kukomesha mgogoro wa ndani nchini Libya na ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura za kukomesha machafuko ya ndani nchini humo.
Libya ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi. Baadhi ya maeneo ya Libya kwa sasa yanadhibitiwa na kundi la kigaidi la Daesh ambalo limetumia vibaya machafuko ya ndani kuimarisah udhibiri wake.