Ethiopia: Wabeba silaha wa Sudan Kusini wameua raia wetu 140
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5260-ethiopia_wabeba_silaha_wa_sudan_kusini_wameua_raia_wetu_140
Serikali ya Ethiopia imesema raia wake 140 wameuawa na kundi la wabeba silaha kutoka Sudan Kusini katika jimbo la Gambela katika mpaka wa nchi mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2016 08:59 UTC
  • Ethiopia: Wabeba silaha wa Sudan Kusini wameua raia wetu 140

Serikali ya Ethiopia imesema raia wake 140 wameuawa na kundi la wabeba silaha kutoka Sudan Kusini katika jimbo la Gambela katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Taarifa ya serikali ya Ethiopia imesema kuwa, uvamizi huo ulifanyika Ijumaa iliyopita katika eneo la Jakaya, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Sudan Kusini na kwamba jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuangamiza wavamizi 60 miongoni mwao. Wakimbizi zaidi ya 284,000 raia wa Sudan Kusini wanaishi katika jimbo la Gambela nchini Ethiopia, lakini haijabainika iwapo uvamizi huo ulitekelezwa na baadhi ya wakimbizi hao. Serikali ya Addis Ababa imesema kuwa, waliohusika na mauaji hayo sio askari wa vikosi vya Sudan Kusini wala waasi wanaoipiga vita serikali ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Taarifa ya serikali ya Ethiopia imesema kuwa, kwa sasa vikosi vyake vinawasaka wavamizi hao ndani ya ardhi ya Sudan Kusini.

Haya yanajiri katika hali ambayo, kongamano la usalama wa bara la Afrika lililoanza jana na linalotazamiwa kumalizika leo katika mji wa Bahir Dar nchini Ethiopia, limejadili changamoto za usalama katika nchi za Afrika. Kongamano hilo la Usalama wa Afrika ambalo ni la tano kufanyika, limehudhiriwa na viongozi mbalimbali wa bara hilo.