Umoja wa Mataifa wamtaka Khalifa Haftar akomeshe mashambulizi dhidi ya Tripoli, Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kundi la G7 limtaka Jenerali Khalifa Haftar akomeshe mashambulizi yake dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Wanamgambo watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar siku ya Alkhamisi walipewa amri na Haftar kwa njia ya mkanda wa sauti ya kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya na jana Ijumaa walifika hadi kwenye lango la kuingilia Tripoli.
Hata hivyo wapiganaji watiifu kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wamesema kuwa wamefanikiwa kuwatia mbaroni zaidi ya wapiganaji 100 wa Jenerali Haftar ambaye amejitangaza kuwa ni mkuu wa Jeshi la Taifa la Libya (NLA).
Mapigano yameripotiwa kushadidi kuanzia jana usiku na hadi leo asubuhi karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli, ulioko umbali wa kilomita 30 kusini mwa mji mkuu huo wa Libya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha faragha cha kujadili mgogoro wa Libya na baada ya kikao hicho lilizionya pande zinazoshadidisha madhafuko huko Libya.
Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelitaka jeshi la Jenerali Khalifa Haftar kukomesha mashambulizi yake na kurejesha nyuma majeshi yake.
Jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres aliitembelea Libya na kuonana na Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, Fayez al Sarraj mjini Tripoli kabla ya kuelekea Benghazi na kuonana na Jenerali Khalifa Haftar. Baada ya mazungumzo hayo, Guterres alisema anaondoka Libya akiwa na huzuni na moyo mzito.