Waziri Mkuu wa Libya: Haftar ametusaliti kwa kuhujumu Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52689-waziri_mkuu_wa_libya_haftar_ametusaliti_kwa_kuhujumu_tripoli
Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj, anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, amemtuhumu hasimu wake, Jenerali Khalifa Haftar kuwa amemsaliti kwa kuanzisha hujuma dhidi ya mji mkuu, Tripoli, jambo ambalo yamkini likaibua vita vya ndani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2019 10:30 UTC
  • Waziri Mkuu wa Libya: Haftar ametusaliti kwa kuhujumu Tripoli

Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj, anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, amemtuhumu hasimu wake, Jenerali Khalifa Haftar kuwa amemsaliti kwa kuanzisha hujuma dhidi ya mji mkuu, Tripoli, jambo ambalo yamkini likaibua vita vya ndani nchini humo.

Al-Sarraj ambaye anaongoza Serikali ya Maelewano ya Kitaifa Libya (GNA) yenye makao yake Tripoli amesema Haftar amewasaliti kwa kuanzisha harakati yake hiyo ya kuipindua serikali.

Wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' (LNA) wanaoongozwa na Haftar wanaripotiwa kufika nje ya mji mkuu Tripoli na kudhibiti uwanja wa zamani wa ndege wa kimataifa. Al Sarraj ameonya kuwa vita hivyo havitakuwa na mshindi. Amesema wametangaza mara kadhaa kuwa wanataka amani lakini kufuatia hujuma ya askari wa Haftar basi hawana budi ila kutumia nguvu kukabiliana nao.

Wanajeshi wa Jenerali Haftar, mwenye makao yake mjini Benghazi, wanaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarrabu na wametumia ndege kushambulia ngome za askari wa serikali ya al-Sarraj.

Jenerali Haftar

Wakati huo huo Jeshi la Serikali ya Maelewano ya Kitaifa (GNA limetangaza kuanzisha oparesheni ya kuulinda mji mkuu Tripoli huku likiapa kuchukua tena udhibiti wa maeneo yote yaliyotekwa na askari wa Jenerali Haftar. Msemaji wa Jeshil la GNA Kanali Mohammad Gnounou amewaambia waandishi habari Jumapili mjini Tripoli kuwa oparesheni hiyo inalenga pia kuwatimua wapiganaji wote haramu kutoka miji yote ya Libya.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.