UN yasikitishwa na hali mbaya ya kibinadamu mjini Tripoli, Libya
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, umoja huo unahuzunishwa mno na hali mbaya ya raia wa Libya katika mapigano yanayoendelea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Stephane Dujarric amesema hayo mjini New York, Marekani na kuongeza kuwa, mapigano katika mji mkuu wa Libya yamezidi kuharibu hali ya kimaisha ya raia wa kawaida huku watu wengi wakizidi kutoa fedha zao benki na wengine wakilimbikiza mahitaji majumbani mwao, suala ambalo limepelekea kupanda vibaya bei za bidhaa.
Msemaji huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, karibu watu elfu 10 wamekimbia makazi yao na kukimbilia nje ya mji mkuu Tripoli kutokana na mapigano hayo. Tayari raia 17 wamesharipotiwa kuuawa katika mapigano hayo.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea pambizoni mwa Tripoli na umeongeza juhudi za kuzipatanisha pande hasimu ili zisimamishe mapigano na hivyo iwezekane kuwafikishia misaada raia waliokimbilia kwenye viunga vya mji mkuu huo wa Libya.
Vile vile amesema, Ghassan Salamé, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya na timu yake bado wako mjini Tripoli na wamepanua wigo wa huduma zao kwa wahanga wa mapigano hayo.
Mapigano mapya yalianza tarehe 4 mwezi huu wa Aprili baada ya wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kuanza kuushambulia mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.