Saudia ilimpa Haftar mamilioni ya dola kabla ya kuanza hujuma Tripoli, Libya
Siku kadhaa kabla ya jenerali muasi Libya, Khalifa Haftar kuanzisha hujuma dhidi ya mji, mkuu wa nchi hiyo, Tripoli, Saudi Arabia ilikuwa imekabidhi mamilioni ya dola ili kutekeleza oparesheni hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imefichuliwa na gazeti la Wall Street Journal toleo la Ijumaa, Haftar alipokea kitita hicho akiwa safarini mjini Riyadh, Saudi Arabia kabla ya kuanzisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Tripoli, tarehe 4 mwezi huu wa Aprili.
Gazeti hilo limewanukulu washauri wa ngazi za juu wa utawala wa Saudia wakisema kuwa Haftar alikubali fedha hizo ambazo amezitumia kuwahonga viongozi wa kikabila, kuwalipa wapiganaji na kwa ajili ya matumizi mengine ya kijeshi.
Hayo yanajiri wakati ambapo Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, umoja huo unahuzunishwa mno na hali mbaya ya raia wa Libya katika mapigano yanayoendelea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli. Stephane Dujarric.
Karibu watu elfu 10 wamekimbia makazi yao na kukimbilia nje ya mji mkuu Tripoli kutokana na mapigano hayo. Tayari raia 17 wamesharipotiwa kuuawa katika mapigano hayo yaliyoanza Apiri Nne.
Wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' (LNA) wanaoongozwa na Haftar wamezusha mapigano makali mjini Tripoli.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Maelewano ya Kitaifa Libya (GNA), Fayez al-Sarraj, anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, amemtuhumu hasimu wake, Jenerali Khalifa Haftar kuwa amemsaliti kwa kuanzisha hujuma dhidi ya mji mkuu, Tripoli, jambo ambalo yamkini likaibua vita vya ndani nchini humo.
Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.