Misri yaunga mkono mashambulizi ya vikosi vya Haftar nchini Libya
(last modified Mon, 15 Apr 2019 08:02:15 GMT )
Apr 15, 2019 08:02 UTC
  • Misri yaunga mkono mashambulizi ya vikosi vya Haftar nchini Libya

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ametangaza kuwa anaunga mkono mashambulizi yanayofaywa na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar yenye lengo la kuudhibiti mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Rais al-Sisi ameyasema hayo alipokutana na  kufanya mazungumzo na Jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar jana Jumapili.

Taarifa ya Ikulu ya Misri imesema kuwa, al-Sisi anaunga mkono kile alichodai kuwa ni jitihada za kupambana na ugaidi na makundi ya wanamgambo yenye misimamo mikali ili wananchi wa Libya wawe na usalama na utulivu.

Rais huyo wa Misri amekuwa mshirika mkuu wa vikosi vya Haftar ambavyo vinadhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa Libya kwa muda mrefu sasa.

Haya yanajiri siku chache baada ya gazeti la Wall Street Journal toleo la Ijumaa kufichua kuwa, Khalifa Haftar alipokea kitita cha mamilioni ya dola akiwa safarini mjini Riyadh, Saudi Arabia kabla ya kuanzisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Tripoli, tarehe 4 mwezi huu wa Aprili.

Wapiganaji wa Khalifa Haftar mjini Tripoli

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO,  mashambulizi ya vikosi vya Haftar vya kutaka kuudhibiti mji mkuu wa Tripoli yamesababisha vifo vya watu 121 na wengine 561 kujeruhiwa. 

Haftar ametupilia mbali wito wa kimataifa unaomtaka asitishe mapigano dhidi ya wapiganaji tiifu kwa serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

 

Tags