Qatar yataka Jenerali Haftar wa Libya awekewe vikwazo vya silaha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ametoa mwito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Jenerali Khalifa Haftar na vikosi vyake vinavyofanya mashambulizi ya kudhibiti mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani aliyasema katika mahojiano na gazeti la Italia la 'La Repubblica' ambalo lilichapisha habari hiyo jana Jumanne na kufafanua kwa kusema, "Kinachopaswa kufanyika ili kuhitimisha mapigano mapya ya Libya ni kumuwekea Haftar vikwazo na kuzizuia nchi ambazo zinampa silaha kuendelea kufanya hivyo."
Amezitaja Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri kama nchi zinazoongoza kumrundikia silaha Khalifa Haftar.
Itakumbukwa kuwa, siku chache zilizopita, gazeti la Wall Street Journal toleo la Ijumaa lilifichua kuwa, Khalifa Haftar alipokea kitita cha mamilioni ya dola akiwa safarini mjini Riyadh, Saudi Arabia kabla ya kuanzisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Tripoli, tarehe 4 mwezi huu wa Aprili.
Aidha Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi alitangaza bayana kuwa anaunga mkono mashambulizi ya vikosi vya Khalifa Haftar, na kwamba eti hizo ni jitihada za kupambana na ugaidi na makundi ya wanamgambo yenye misimamo mikali ili wananchi wa Libya wawe na usalama na utulivu.
Rais al-Sisi aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar siku ya Jumapili.
Huku hayo yakijiri, Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulizi ya vikosi vya Haftar vya kutaka kuudhibiti mji mkuu wa Tripoli imeongezeka na kufikia watu 147 huku wengine 614 kujeruhiwa.