Elfu 18 wakimbia mapigano Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52900-elfu_18_wakimbia_mapigano_libya
Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba watu wasiopungua 18,000 wamekimbia mapigano makali yanayoendelea kati ya jeshi linalojiita kuwa la kitaifa na la serikali ya muungano wa kitaifa huko Tripoli nchini Libya
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 17, 2019 07:23 UTC
  • Elfu 18 wakimbia mapigano Libya

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba watu wasiopungua 18,000 wamekimbia mapigano makali yanayoendelea kati ya jeshi linalojiita kuwa la kitaifa na la serikali ya muungano wa kitaifa huko Tripoli nchini Libya

Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa huku akilinukuu Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM amesema kwamba watu 614 wakiwemo raia 35 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ambapo 174 wakiwemo raia 13 wamepoteza maisha katika mapigano hayo. Ameongeza kwamba idadi ya raia waliouawa katika mapigano hayo ni kubwa kuliko ile iliyotangazwa rasmi katika vyombo vya habari. Kwa mujibu wa Dujarric, kuna karibu watu 3000 wanaoendelea kushikiliwa katika vituo tofauti karibu na maeneo ya mapigano.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa

Amesema katika baadhi ya sehemu, walinzi wa vituo hivyo wamewaacha wakimbizi bila ya kuwapa suhula zozote za msingi kama vile chakula na maji. Ripoti zinaeleza kuwa kuendelea mapigano hayo pambizoni mwa mji wa Tripoli huenda kukawasha vita vya ndani kama vile vilivyoshuhudiwa  mwaka 2011 na ambavyo vilipelekea kung'olewa madarakani na kisha kuuawa kwa Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya. Mapigano ya hivi karibuni nchini humo yalianza tarehe 4 mwezi huu kufuatia safari ya Khalifa Haftar kamanda wa jeshi la kitaifa la Libya nchini Saudia, ambapo mara tu baada ya kurejea nchini alitangaza vita dhidi ya Tripoli, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo.