Libya yaituhumu Ufaransa kuwa inachochea vita nchini humo kwa kumuunga mkono Haftar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52941-libya_yaituhumu_ufaransa_kuwa_inachochea_vita_nchini_humo_kwa_kumuunga_mkono_haftar
Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa inaituhumu serikali ya Ufaransa kuwa inahusika katika kuchochea mapigano makali yanayoshuhudiwa katika nchi hiyo hiyo ya kaskazini mwa Afrika
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 19, 2019 03:22 UTC
  • Libya yaituhumu Ufaransa kuwa inachochea vita nchini humo kwa kumuunga mkono Haftar

Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa inaituhumu serikali ya Ufaransa kuwa inahusika katika kuchochea mapigano makali yanayoshuhudiwa katika nchi hiyo hiyo ya kaskazini mwa Afrika

Katika taarifa Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Ndani Fathi Bashagha amesema Ufaransa inamuunga mkono jenerali muasi Khalfa Haftar mwenye makao yake katika mji wa Benghazi, magharibi mwa Libya, na ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kijeshi ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli.

Kwa msingi huo Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya (GNA), yenye makao yake Tripoli na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa sasa imeamua kukata uhusiano wake na Ufaransa.

Haftar pia anapata uungaji mkono wa tawala za Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia. Katika upande mwingine, Italia, ambayo ilikuwa mkoloni wa Libya, inaiunga mkono serikali ya Tripoli na imekasirishwa na hatua ya Ufaransa ya kukataa kuidhinisha azimio la Umoja wa Ulaya la kumtaka Haftar asitishe hujuma yake Tripoli. Wakati huo huo Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya imetoa waranti wa kukamatwa Haftar na maafisa wake sita kwa kuhusika katika hujuma dhidi ya maeneo ya raia.

Shirika la Afya Duniani linasema kwa uchache watu 205 wamepoteza maisha tokea Aprili 4 wakati Haftar alipoanzisha oparesheni yake ya kutaka kuuteka mji wa Tripoli.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.